News
Loading...

HALI YA WAISALAM TANZANIA

Uthibitisho wa njama dhidi ya Waislamu nchini
HII ni sehemu ya kumi ya mfululizo wa makala ambazo ni sehemu ya muswada wa kitabu "Mwalimu Julius K. Nyerere, Kanisa Katoliki na Uislamu: Dola na tatizo la Udini Tanzania" kitakachotoka hivi karibuni. Kitabu hicho kimeandikwa na mwandishi maarufu wa masuala ya historia hasa ya Tanganyika BWANA MOHAMMED SAID.
KWA nchi ambayo inajigamba kuwa inajali usawa kwa wananchi wake inashangaza kuona kuwa Waislamu wanabaki nyuma na juhudi zozote ambazo Waislamu watafanya ili kuondoa upogo kati yao na Wakristo na kujiletea maendeleo zinapata upinzani na uadui kutoka na mfumo ule ule unaojidai kuwa unasimamisha usawa na haki.
Kitu cha kusikitisha ni kuwa hakupata kusimama hata Muislamu mmoja katika wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM kumuunga mkono Profesa Malima kwa dhulma ambayo wote walikuwa wanafahamu kuwa imedumu kwa kipindi kirefu. Hata ndani ya Bunge hakuna Muislamu aliyekuwa na ujasiri wa kumtetea Profesa Malima. Muislamu mmoja, Mwenyekiti wa Mkoa wa Pwani, Masudi Mtandika, aliungana na kambi ya Wakristo katka Kamati Kuu ya CCM kumshambulia Profesa Malima. Msimamo wa Mtandika ulikuwa sawa na ule wa Rajab Diwani na Selemani Kitundu walipomshambulia Bibi Titi Mohamed wakati Kamati Kuu ya TANU ilipokuwa ikijadili EAMWS mwaka wa 1963.
Kampeni ya chuki na propaganda dhidi ya Profesa Malima ikaanzishwa na vyombo vya habari ambavyo vyote vilikuwa chini ya miliki ya Wakristo na hivyo chini ya Kanisa.
Aboud Jumbe, rais wa zamani wa Zanzibar na Makamu wa Rais wa Tanzania, amefanya utafiti kuhusu nafasi ambazo wameshika Waislam katika serikali, Bunge na vyuo vya elimu ya juu. Takwimu alizoonyesha Aboud Jumbe zinatisha. Katika baadhi ya taasisi Waislamu wanaonekana kwa kutokuwepo katika taasisi hizo. Utafiti wa Jumbe ulikuwa wa pili katika kueleza tatizo hili la Waislamu na kuliweka wazi kwa matumaini ya kuwa labda serikali ingeweza kuhisi kuwajibika na kujaribu kusahihisha makosa hayo.
Majaribio mengine yamewahi kufanyika huko nyuma na watu kama Sheikh Abubakar Mwilima, wakati huo akiwa Mwenyekiti wa JUWATA na katika Kamati Kuu ya chama tawala CCM, alijaribu kuieleza serikali tatizo hili la Waislamu.
Kitu kimoja mashuhuri kwa wote waliojaribu kuliweka tatizo hili mbele ya serikali wote hao walimalizwa kisiasa. Maisha yao katika siasa yalikatizwa ­ Chifu Abdallah Said Fundikira, Tewa Said Tewa, Bibi Titi Mohamed, Mufti Sheikh Hassan bin Amir, Mussa Kwikima, Sheikh Abubakr Mwilima, Profesa Kighoma Malima na wengine wengi. Ilikuwa kuanzia hapa ndipo Waislamu walianza kunong'ona kuhusu njama dhidi yao.
Kuwepo kwa njama dhidi ya Waislamu kulikuja kudhihirishwa pale watafiti wa Kikristo walipoanza kufanya utafiti kuhusu athari za Ukristo katika utawala wa dola; na bila kujali matokeo ya utafiti kwa hisia za Waislamu wakawa wanaeleza jinsi Waislamu kwa hila na msaada wa serikali walivyowekwa pembeni katika kugawana madaraka na Wakristo.
Hivi sasa kuna vitabu viwili vilivyoandikwa na Wakristo wenyewe vinavyothibitisha kuwa Wakristo wametumia nyadhifa zao katika serikali kuuhujumu Uislamu na Waislamu.
Jan P van Bergen katika kitabu chake, Development and Religion in Tanzania, (1981) ametoboa siri kuhusu uadui aliokuwa nao Nyerere dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Kitabu kinaeleza kwa ufasaha jinsi Nyerere wakati alipokuwa madarakani alivyokuwa akifanya mikutano ya siri na viongozi wa Kanisa kuweka mikakati ya kuupa nguvu Ukristo. Katika mikutano hiyo Nyerere aliwahakikishia viongozi wa Kanisa kuwa anaaunga mkono Ukristo.
Kitabu hicho kinaeleza jinsi Nyerere alivyotimiza ahadi yake hiyo kwa Kanisa kwa kuhakikisha kuwa anawapa Wakristo nafasi za juu katika serikali na chama.
Kitabu hiki kilikuwa kikiuzwa Catholic Bookshop, Dar es Salaam. Lakini ilipokuja kudhihirikia Kanisa kuwa kitabu hiki kilikuwa kinatoa habari nyeti na siri za Kanisa kuhusu njama dhidi ya Waislam, kwa haraka sana kikaacha kuuzwa. Hadi hivi sasa kitabu hicho ni marufuku kuletwa tena Tanzania.
Kitabu cha pili ni cha Dr John C. Sivalon, Kanisa Katoliki na Siasa ya Tanzania Bara 1953 Hadi 1985 (1992).
Kitabu hiki kinaeleza njama ndani ya serikali kuuhujumu Uislam. Sivalon anafichua kuwa kuanzia mwaka 1961 baada ya Tanganyika kupata uhuru, Kanisa lilikuwa na hofu mbili. Hofu ya kwanza ilikuwa umoja wa madhehebu za Kiislamu kati ya Sunni, Bohora, Ismailia na Ithnasheri. Hofu ya pili ilikuwa kuhamishwa kwa makao makuu ya EAMWS kutoka Mombasa kuja Dar es Salaam. Kanisa lilikuwa linahofu kuwa mali walizokuwanazo Waasia Waislamu zikitiwa katika shughuli za Waislamu ambao walikuwa na nguvu kubwa katika uwanja wa siasa zitaathiri maslahi ya Ukatoliki katika Afrika ya Mashariki. Kwa ajili hii Kanisa likatanganza kuwa Uislamu ni adui wake na ikaanza mikakati ya hujma dhidi ya Uislamu ili kuudhoofisha.
Kuna kazi mbili zilizoandikwa na Waislamu kuhusu uhusiano baina ya serikali na Waislamu. Kazi ya kwanza ni tasnifu ya Kiwanuka, 'The Politics of Islam in Bukoba District' (1973); kazi ya pili ni makala ya utafiti 'Islam and Politics in Tanzania' (1989) iliyoandikwa na mwandishi wa kitabu hiki.
Ilikuwa baada ya kusoma tasnifu ya Kiwanuka na kuona jinsi ukweli wa kuvunjwa kwa EAMWS kulivyopoteshwa ndipo kama Muislamu na kama ada ya Uislamu inavyodai kuwa pande mbili za mgogoro zote lazima zisikilizwe, ndipo nilipoamua kufanya utafiti na kuandika tatizo lile kwa mtazamo wa Waislamu. Ukweli ambao kwa miongo miwili ulizuiwa usifahamike kwa Waislamu.
Kiwanuka anadai na kuafiki kuwa Nyerere alikuwa na haki ya kutumia vyombo vya dola dhidi ya Waislam kwa kuwa kama asingefanya hivyo nchi ingekuwa na mamlaka mbili, yaani ya Waislam na ya serikali. Kwa ajili hii aliamua kuivunja EAMWS ili 'kulinda umoja wa kitaifa'.
Halikadhalika ipo 'Kwikima Report' (1968) ambayo imeeleza kwa ufasaha tatizo la EAMWS, chanzo chake na mchango wa serikali katika kuhujumu umoja wa Waislamu. Taarifa hii inafaa kutumika leo kama dira ya kuelewa tatizo la Waislamu wa Tanzania kama ilivyokuwa wakati ule ilipotolewa kwa mara ya kwanza.
Taarifa ya Kwikima inaeleza jinsi TANU, serikali na Waislam wachache katika TANU walivyodanganyika kudhani kuwa katika kuisaidia serikali kuivunja nguvu EAMWS walikuwa wanatimiza uzalendo na maslahi ya taifa.
Rejea hizi tano ni muhimu kwa wanafunzi wa historia ya siasa Tanzania; na kwa mtafiti yeyote anaetaka kujua chanzo cha chuki baina ya Waislam na serikali na chanzo cha hisia kali za kidini zinazoikumba nchi yetu kuanzia miaka ya 1980.
Rejea zote hizo za vitabu, makala za utafiti na taarifa mbalimbali, ingawa zimeandikwa na waandishi tofauti na kwa muelekeo tofauti zote hizi zinadhihirisha kitu kimoja ­ kuwepo kwa njama zinazoendelea kwa zaidi ya karne moja dhidi ya Uislamu na Waislamu, kwanza zilikuwa zikifanywa na wakoloni walioitawala Tanganyika na sasa zinafanywa na Wakristo wananchi kuhakikisha kuwa Uislamu haupati nguvu. Kama hali ndiyo hii vipi Uislamu hadi leo bado upo Tanzania na unazidi kupata nguvu kila kuchao? Jibu lipo ndani ya Qur'an.
Hivi sasa Waislamu wanamshutumu Mwalimu Nyerere na uongozi wa Kanisa kwa kusaliti dhamana aliyokabidhiwa na Waislamu ambao ndiyo waliopigania uhuru wa Tanganyika.
Waislamu wa Tanzania hivi sasa ni kama wanazaliwa upya. Kila kukicha wanatafakari hali yao na mustakbali wao katika Tanzania huru Walipambana na wakoloni, kuanzia vita vya Maji Maji mwaka 1905 hadi kuanzishwa kwa African Association mwaka 1929 na TANU mwaka 1954; hadi uhuru ukapatikana mwaka 1961.
Waislamu wanaamini kuwa baadhi ya majibu ya matatizo yanayowakabili hivi sasa yapo kwenye hii historia yao ya kudai uhuru. http://kiswahili.irib.ir/media/k2/items/cache/5510bab8e49968c660177ec33ba21035_XL.jpg
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment
    Facebook Comment

0 comments :

Post a Comment